Wasifu wa Haji Gora Haji

Wasifu wa Haji Gora Haji

Adriana Gabriela Bañales De León

Haji Gora Haji ni mshairi Mtanzania mwenye maarufu huko nchini Tanzania, hasa katika visiwa vya Zanzibar, lakini Haji ni mwanamuziki, mwandishi na msimulizi wa hadithi na mashairi pia. Haji Gora alizaliwa tarehe kumi, mwezi wa tatu, mwaka elfu moja mia tisa thelathini na tatu kisiwani Tumbatu. Haji alipokuwa na umri wa miaka mitano, familia yake yote naye walihama kuelekea mji wa Zanzibar.

Familia nzima ya Haji ilikuwa kubwa na hawakuwa na pesa nyingi; Haji ana ndugu tano na wandugu wa kambo kumi na moja. Ndivyo haikuwezekana kumlipia Haji elimu yake, kwa hivyo alijifunza hila rasmi ya familia yake yaani: kuvua samaki. Hilo lilimruhusu awe mtaalamu wa bahari. Wakati huo shule za Kurani tu zilikuwa bure, kwa hivyo Haji alipokuwa na umri wa miaka saba alianza elimu yake katika shule ya Kiislamu. Huko alijifunza mashairi ya kidini yaliyoandikwa kwa Kiswahili yaliyofuata mfumo wa jadi wa mashairi ya Kiarabu. Mashairi hiyo yanasifika kwa kufuata mahadhi yanayokuwa makali sana. Kama wanaume wengi katika Afrika ya Mashariki, Haji ana wake zaidi ya mmoja na anao watoto kumi na nne.

Mnamo mwaka elfu moja mia tisa hamsini na tano, Haji alitunga wimbo wake wa kwanza, alipokuwa mwanachama wa kundi la kuimba na kucheza dansi lililogombea katika mashindano ya heshima ya Tumbatu. Kwa hivyo wimbo huo ulikuwa unahusiana na kisiwa cha Tumbatu na uzuri wake. Kuanzia wakati hiyo Haji alijulikana kama msemaji mmoja mkuu wa mashairi na nyimbo katika lugha za Kiswahili na Kitumbatu, ambacho ni lugha ya mama yake. Mashairi yake kadhaa yameshaandikwa katika lugha hizo zote mbili. Mwaka elfu moja mia tisa tisini na nne Haji alichapisha kitabu chake cha mashairi, kinachoitwa Kimbunga. Kutokana na umaarufu wa kitabu hiki Haji alipata umashuhuri mjini Zanzibar na pia kitabu hiki kimetafsiriwa katika Kiingereza, Kifaransa na Kiholanzi.

Ingawa watu wengi wanadhani kwamba shairi la “Kimbunga” linaelezea uharibifu ambao kimbunga kilisababisha, Haji amefafanua kwamba shairi hilo linahusiana na ukatili uliofanyika katika mapinduzi ya Zanzibar mnamo mwaka elfu moja mia tisa sitini na nne. Kwa njia ya kutumia mafumbo, shairi hili linakitaja Chama cha Afro-Shirazi1 na Ushirikiano wa Tanganyika wa Umoja wa Kitaifa. Pia linamkumbusha msomaji historia kuhusu Zanzibar na mabadiliko yote ambayo mapinduzi yalisababisha katika maisha ya wananchi wa kisiwa hiki (Lichtenstein 2012).

Mwaka elfu mbili na tisa Haji alichapisa kitabu chake cha pili, kinachoitwa Siri ya Gining’i. Pia Haji alishiriki katika tamasha za mashairi katika miji kadhaa, kwa mfano mjini Medellin nchini Colombia na mjini Rotterdam huko Uholanzi. Mara kwa mara Haji amechangia katika vipindi vya maandishi katika redio ya Tanzania na pia yeye ni mwanachama wa kamati za lugha ya Kiswahili (Samsom 2002). Vilevile Haji anafurahia kusoma mashairi ya waandishi wengine kutoka nchi mbalimbali.

Sasa, mashairi na hadithi ya Haji Gora hutumika shuleni Tanzania, lakini hajapata faida nyingi kwa maandiko yake ambayo yamechapishwa; Haji amesema kwamba ameshapata dola mia mbili tu (Lichtenstein 2012). Kwa vyovyote yeye ameamua kwamba hataacha kutunga mashairi kamwe. Haji amejitolea zaidi ya miaka arobaini kwa kuandika fasihi simulizi, mashairi na hadithi na inaonekana hakuna kitu kinachoweza kumsababisha aache.

Marejeo


1Chama cha Afro-Shirazi (ASP, akronimi katika Kiingereza) kilikuwa muungano wa vyama vya Shirazi na vyama vya Waafrika vilivyokuwa Zanzibar. Wakati wa mapinduzi ya Zanzibar, ASP pamoja na Ushirikiano wa Tanganyika Wa Umoja wa Kitaifa (TANU, akronimi katika Kiingereza) waliangusha serikali ya Waarabu ilioongozwa wa Jamshid bin Abdullah na waliumba Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Baada ya miezi michache, Jamhuri hii iliungana na Tanganyika ili kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

*Esta web está en continuo desarrollo, siendo actualizado su contenido periódicamente, por lo que progresivamente va ampliando el material publicado. 

colmex-swahililogo ceaa 50 

© 2015 El Colegio de México, A.C.