Skip to main content

Siku ya Wahenga nchini Mehiko

Siku ya Wahenga nchini Mehiko

18. Mazoezi ya Kusikiliza (Comprensión Oral) 3

Adriana Franco Silva

Mara moja kwa mwaka Wamehiko wanatarajia kutembelewa na wahenga wao. Matembezi hayo yanatokea tarehe mbili, mwezi wa kumi na mbili. Wamehiko wanasherehekea siku hiyo kwa furaha na heshima kwa mizimu yao. Chanzo cha desturi hii kinaweza kupatikana katika mila za wenyeji wa Mesoamerika zilizohusiana na wahenga wao marehemu. Pamoja na hayo, desturi hizo zilichanganyika na mawazo ya Wahispania.

Inajulikana kwamba Waamerika wa kizamani waliwasujudu wahenga wao mara kadhaa katika mwaka mzima. Pia wao walikuwa na miungu waliowakilisha kifo, kwa mfano Mictlantecuhtli, aliyesindikiza mizimu katika safari yao kuzimuni (Del Moral 2000, 39). Mictlantecuhtli, aliyefikiriwa kama kiunzi cha mifupa chenye madoadoa ya rangi ya kimanjano, alitawala Mictlan, mahali ambapo wahenga marehemu walikaa baada ya kufa.

Wakati Wahispania walipofika bara la Amerika makahini wa kanisa ya katoliki waliamua kutumia baadhi ya mila hizo walizokuta huko ili wenyeji wasiliki kanisani mwao na kwa ajili ya kubadilisha desturi za wenyeji wa Amerika. Wahispania walikuwa na mawazo yaliyofanana na mila za Waamerika, kwa mfano “siku ya waroho wote” au “siku ya wahenga waaminifu”, ingawa wao walizisherehekea kwa njia tofauti. Sasa Wamehiko wanachosherehekea ni matokeo ya mchanganyiko huo.

Sifa moja ya sherehe hii, na mojawapo inayojulikana mno, ni sadaka. Kwa ujumla, watu wanaweka sadaka mezani. Meza hii inapambwa na karatasi za mapambo; cempasúchil, ambayo ni maua ya rangi ya kimanjano au ya machungwa; maji ili wahenga wasiwe na kiu; chakula ambacho wao walipenda sana walipokuwa hai na pengine pombe kali. Pamoja na hayo kunawekwa peremende za kienyeji kama “calaveritas” ambazo ni peremende za sukari au chokoleti zenye umbo wa fuvu la kichwa. Zaidi ya hayo, watu wanaweka mishumaa kwa ajili ya kuongoza njia ambayo wahenga wanaelekea na pia wanaweka picha zao. Sadaka inaweza kuwa na vitu vingine lakini hivyo vilivyotajwa ni vya kawaida.

Tarehe ya sherehe hiyo ikikaribia waokaji wanaanza kuoka “mkate wa wahenga”. Mkate huo una muundo wa mduara na juu ya huu kuna mistari minne inayoungana na mpira mdogo. Umbo huo unawakilisha fuvu la kichwa na mifupa. “Mkate wa wahenga” ni mtamu na watu wanaweza kuonja ladha ya maua ya machungwa wanapoula.

Baadhi ya watu wanaenda kwenye makaburi ya wahenga marehemu ili washerehekee pamoja nao. Kwa ukweli, inasemekana kwamba makaburini kunajaa furaha na uhai. Watu wanaofuata desturi hii wanakesha usiku kucha makaburini mwa wahenga wao. Wao wanabeba chakula na kinywaji ili wale na wanywe pamoja na wahenga wao, pia wanazungumza nao kiroho. Mahali mbili zinazotukuka kwa ajili ya mila hii ni makaburi ya San Andrés Mixquic yapatikanayo ukingoni mwa mji wa Mehiko na Pátzcuaro, jimboni Michoacán.

  1. Wamehiko wanasherehekea “Siku ya wahenga” tarehe ngapi na wanangoja nini itokee siku hii?
  2. Shina la sherehe hiyo ni nini?
  3. Nani aliwasindikiza wahenga katika safari yao kuzimuni?
  4. Aliyetawala Mictlán ni nani?
  5. Kwa nini Wahispania walitumia baadhi ya desturi za wenyeji wa Amerika ambapo walifika bara hili?
  6. Kwa ujumla, ni vitu gani ambavyo watu wanaweza kuweka katika sadaka ya “siku ya wahenga”?
  7. Waokaji wanaoka nini kwa ajili ya sherehe hizo? Eleza muundo na ladha zake.
  8. Kwa nini inasemekana kwamba makaburi yanajaa furaha na uhai siku ya wahenga?
  9. Taja mahali mbili zilizo na maarufu katika kusherehekea siku hii.
  10. Je, kuna sherehe kama hiyo nchini kwako?

Marejeo

  • Del Moral, Raúl, “En torno a Mictlantecuhtli”, Estudios Mesoamericanos, 1, 2000.