Mazoezi ya Kusikiliza (Comprensión Oral) 2

Son Jarocho, muziki wa Veracruz

Adriana Gabriela Bañales De León

Veracruz ni jimbo la Mehiko ambalo liko mashariki na pwani. Jimbo hili limebarikiwa tamaduni nyingi za aina mbalimbali, hasa utamaduni wa Hispania, na ule wa watumwa walioletwa kutoka Afrika pamoja na watu wa kienyeji wa mkoa huo waliokuwepo kabla yao. Kwa hivyo muziki wa Veracruz ni matokeo ya mchanganyiko huo. Muziki huu unajulikana kama son jarocho. Neno la “son” linamaanisha “sauti ambayo ni nzuri kwa sikio” (Sheehy aliyetajwa kwa Loza 1992, 179) na linatokana na neno la Kilatini sonus (Stanford 1972, 66). Watu wanaotoka Veracruz kwa ujumla wanajulikana kwa jina la “jarocho”.

Son Jarocho inasifika kwa mashairi yake na kwa kutumia vyombo vya muziki kama vile jarana, requinto na leona ambazo ni aina mbalimbali za magitaa zinazotengenezwa kutokana na gitaa za Kihispania. Pia inawezekana wanamuziki watumie fidla na aina ya sanduku inayotumika kama ngoma ya Hispania inayoitwa cajón. Mara kwa mara wanatumia kinubi kikubwa. Muziki huo ulitumia ngoma kadhaa, lakini wakati wa ukoloni Wahispania walikataza ngoma. Hilo lilisababisha kwamba ngoma ziliondolewa na watu walianza kucheza dansi juu ya tarima, yaani sanduku ya mbao, kwa hivyo watu wengi wanafikiri kwamba dansi hii ni kama kupiga ngoma kwa miguu. Dansi ile inaitwa zapateado na inafanana na dansi ya flamenco ya Hispania, kutokana na jinsi michezo inavyofanana, Wahispania hawakuweza kuwakataza watu wacheze zapateado.

Wakati wa Upelelezi Takatifu huko Hispania, Wahispania waliwakataza watu wacheze son jarocho kwa sababu mashairi yake yalifikiriwa kuwa zinifu na ya kufuru. Hilo ni kwa sababu mara kwa mara mashairi hayo yanahusiana na hali za pyororo na utani (Loza 1992, 179-180). Sawa na jinsi yalivyo katika mahali mengi huko Afrika, mashairi mengi ya muziki wa son jarocho hayajaandikwa, Jimboni Veracruz watunzi hutunga mashairi yao kwa ghafla, hasa wakati wa sherehe za son jarocho zinazoitwa fandango. Sasa mashairi hayo yanahusiana na mapenzi, uzuri wa jimbo la Veracruz (Reuter 1968, 34) na maisha ya kila siku ya Wajarocho, hususa watu wanaoishi kusini ya jimbo hilo.

Kwa kawaida sherehe hizi zinafanyika wakati wa usiku na watu wote wa mtaa wanajitahidi kushiriki; watu wengine wanaweza kucheza dansi ya zapateado, wengine wanapiga jarana, cajón au fidla na wengine wanaimba na kutunga mashairi. Washiriki wote wanatabaruki karibu ya tarima. Katika fandango kuna vyakula vingi vya Mehiko, kwa mfano tamales na pia kuna pombe kali na maji ya matunda.

Kila mwaka, watu wengi kutoka nchi nzima wanasafiri kuenda mji wa Tlacotalpan, karibu na mto wa Papaloapan, kwa sababu kunafanyika Mkutano wa Kitaifa Wawapiga jarana. Siku tatu nzima mfululizo, mji huu unajaa muziki, vicheko na dansi. Sherehe hii inafanyika wakati wa maadhimisho ya kikatoliki ya Candelaria katika mji huo, ambayo ni tarehe mbili, mwezi wa pili. Kufuatana na umuhimu wa sherehe hiyo na umashuhuri wa son jarocho, watu wengine wamefikiri kwamba muziki huu ni muziki wa kitaifa ya nchi nzima.

Maswali:

  1. Jina linalotumika kwa watu wanaotoka jimbo la Veracruz ni jina lipi?
  2.  Kwa nini muziki wa son jarocho ulikatazwa na Wahispania wakoloni?
  3. Mkutano wa kitaifa wa wapiga jarana unafanyika wapi?
  4. Neno la “son” linamaanisha nini?
  5. Muziki wa Veracruz ni matokeo ya mchanganyiko gani?
  6. Inaitwaje muziki wa jimbo hilo?
  7. Maadhimisho ya kikatoliki ya Candelaria yanafanyika tarehe gani?
  8. Kwa nini dansi ya zapateado haikukatazwa na Wahispania?
  9. Mashairi wa son jarocho kwa kawaida yanahusiana na nada gani?
  10. Vyombo vya son jarocho vinavyopigwa ni vipi?

Marejeo:

  • Loza, Steven. “From Veracruz to Los Angeles: The Reinterpretation of the ‘Son Jarocho’”. Katika Latin American Music Review. Vol. 13. No. 2. University of Texas Press 1992. Pp. 179-194.
  • Reuter, Jas. “El son jarocho”. Katika Diálogos: Artes, Letras, Ciencias humanas. Vol. 4. No. 5. El Colegio de México. 1968. Pp. 33-34.
  • Stanford, E. Thomas. “The Mexican Son”. Katika Yearbook of the International Folk Music Council. Vol. 4. 25th Anniversary Issue. International Council for Traditional Music. 1972. Pp. 66-86.

*Esta web está en continuo desarrollo, siendo actualizado su contenido periódicamente, por lo que progresivamente va ampliando el material publicado. 

colmex-swahililogo ceaa 50 

© 2015 El Colegio de México, A.C.