“Kunganyira” ni hadithi iliyotungwa na Haji Gora Haji na ilichapishwa mwaka elfu mbili na nne. Hadithi hii inahusiana na uroho na mambo mabaya ambayo huletwa nao. Hadithi inatokea katika kijiji kinachoitwa “Nipe Nikupe”, jina linaloonyesha kwamba watu wanaoishi huko walikuwa na ukarimu, lakini mhusika mkuu wa hadithi hii, aitwaye Kunganyira, ana tofauti kubwa nao. Hadithi nzima inahusiana na matendo na mawazo mabaya ya Kunganyira, lakini mwishowe yeye anajifunza kwamba uchoyo humletea hasara. Kunganyira siyo mtu mmoja pekee atakayejifunza somo hili. Pia watu wote wasomao hadithi ya Haji wataelewa jambo kwa sababu hiyo ina maadili na mafundisho yenye maana.
Msingi wa kijiji “Nipe Nikupe” ni utaratibu wa kugawiana na huko kila mtu anawajua wanakijiji wengine wote. Kitendo cha kugawiana kinahusishwa na mtazamo wa makundi ya Waafrika wengi, ambapo umma ni muhimu zaidi kuliko ubinafsi. Kwa sababu hii, watu wa kijiji hiki wanagawiana chakula chao. Hivyo, kama mtu asipokuwa na nyama, watu wengine wa jamii watampa anachohitaji. Kitendo hicho kinafanyika kwa ajili ya manufaa ya umma kwa jumla, kwa sababu inadhaniwa kwamba mtu si mtu bila jamii.
Huko zamani “Nipe Nikupe” kilikuwa kidogo sana, kwa hivyo kila mtu alifahamu mahali ambapo wengine walikuwa hawana chakula au walipokuwa wagonjwa. Watu wa kijiji hiki walikuwa wawindaji na wao wote waligawiana wanyama waliowinda ambapo jirani au familia nyingine walihitaji kitoweo. Kunganyira alikuwa mwindaji bila hodari na alikuwa na watoto wengi waliokuwa wanapenda sana nyama na walipigania chakula kama paka wenye njaa, kwa hivyo Kunganyira alitegemea ukarimu wa wanakijiji daima.
Kwa sababu hii, Kunganyira alipenda sana utaratibu wa kugawiana wa kijiji chake, lakini alitaka pia angalikuwa mwindaji mwenye hodari ili awalishe watoto wake. Siku moja alimkamata kanga wa porini na alikuwa anafurahi sana, lakini alianza kuwa na mawazo ya kiroho. Kunganyira hakutaka jirani zake wafahamu kuwa yeye alikuwa amemkamata kanga huyu na kwa hivyo alimwambia mkewe mpango wake wa kumficha kanga na kutogawia kitoweo. Kunganyira alifikiri kwamba hicho sicho kibaya kwa sababu familia yake ilikuwa kubwa sana na angewagawia wenzake wote nyama ya kanga isingetosha ili awalishe watoto wake. Ingawa mawazo yake yanaweza kudhaniwa kuwa halali, ukweli ni kwamba Kunganyira alipatwa na uroho na pia wakati huo alisahau kwamba marafiki zake walikuwa wamemsaidia ili kuwaletea yeye na familia yake chakula kila mara.
Kunganyira alimficha kanga ndani ya kinu. Mkewe alienda dukani na yeye Kunganyira aliamua kuwaambia watu wa “Nipe Nikupe” kwamba utaratibu wa kupeana vitoweo umalizike mara moja. Baada ya Kunganyira kuwaambia hayo wanakijijij walikuwa na uhakika kwamba Kunganyira alikuwa amempata mnyama mkubwa na hakutaka kugawiana nao nyama aliyopata. Wakati huo huo msichana mmoja alienda nyumbani kwa Kunganyira ili akope kinu, lakini kwa vile kulikuwa hakuna mtu aliamua kuingia na kukichukua. Msichana alipojaribu kuchukua kinu hicho, kanga aliruka na kuponyoka. Kwa hivyo Kunganyira aliporudi kanga alikuwa ameshaondoka.
Kunganyira hakuweza kuamini na wasiwasi ilimjaa. Baadaye mkewe alirudi na Kunganyira alimweleza habari baya iliyokuwa imetokea. Mkewe alikuwa na wasiwasi sana kwa sababu alijua kwamba hakuna mtu atakayetaka kuwagawia kitoweo na watoto wake watalala njaa. Kunganyira alisikitika na kuwaomba watu samaha, lakini wanakijiji waliamua kumpa fundisho na hawakugawia kitoweo naye hadi tabia yake ya uhoro ibadilishwe kuwa tabia ya ukarimu.